Hotuba ya M. Stolz – VETA-Mwanza Julai 2010

Hotuba ya Michael Stolz, VETA – Mwanza Julai 2010

Wanafunzi tisa ya Shule ya Domestic Science, Wuerzburg waliwatembelea wenzao wa VETA-Mwanza mwezi wa Julai 2010 wakiongozwa na Mwl. Michael Stolz aliye mwenyekiti wa MWANZA-Association, Wuerzburg.

Waheshimiwa mabibi na mabwana!

Awali ya yote napenda kuwashukuru sana wenyeji wetu wa VETA kwa mapokezi mazuri mliyotupatia. Napenda kumshukuru Mkuu wa Chuo, ndugu Theobald Titus Isaka. Licha ya kuwa mpya katika wajibu huu amesaidiana nasi bega kwa bega kufanikisha ziara hii. Najua kuwa ndugu Isaka ni rafiki wa udugu wetu kati ya Würzburg na Mwanza. Napenda kumshukuru Registrar Dorothy Kihampa, ambaye toka mwanzoni amesaidiana nasi kuandaa ziara yetu. Namshukuru pia mwalimu Joyce, ambaye bila shaka siku zijazo atasumbuliwa vya kutosha nasi.

Naomba sasa niutambulishe ujumbe wetu kifupi:

Huyu ni Doris Mehling, Profesa maarifa ya nyumbani. Alilipokea mara moja wazo la kutembelea Mwanza na kufanya lolote aliloweza kufanikisha safari hii. Huyu ni Homaira Mansury, Mwalimu wa Academy ya Frankenwarte. Yeye pia ametusaidia sana kufanikisha msafara wetu. Aliendesha semina ya kuwaanda wanafunzi hawa kuja huku.

Mimi mwenyewe ni Mwenyekiti wa M.W.A.N.Z.A, kikundi kilichosajiliwa rasmi na serikali yetu. Lengo letu ni kufanya udugu wa miji yetu uwe hai na udumu. Mwezi Novemba mwaka jana nilikuwa hapa pamoja na kwaya ya VOICES toka Würzburg. Tulifanikiwa kutuimbuiza mahali mbali mbali kama vile Furahisha Open Space.

Wasichana hawa wanatoka kwenye familia za kawaida kabisa na hawakuwa na fedha kugharimia safari ndefu kama hii. Ndiyo maana tulilazimika kutafuta wafadhili waliotusaidia kufanikisha ziara hii.

Tumepewa mahali pazuri sana pa kulala hapa – tunajisikia kuwa kama ujumbe rasmi wa serikali! Safari yetu ilikuwa nzuri. Wote wameguswa sana na uzuri wa mji wa Mwanza na mazingira makubwa na mazuri ya VETA.

Ukiacha mimi, wote wanatembelea kwa mara ya kwanza kabisa Afrika kusini ya Sahara. Mishangao mishangao ya mwanzoni sasa imepita na wote wanafurahia na kungojea kwa hamu mambo mengi watakayoyaona na kujifunza hapa.

Ni mara ya kwanza kabisa kwa wanafunzi wa maarifa ya nyumbani toka Würzburg kukutana na wanafunzi wenzao hapa Mwanza. Nina hakika kabisa kwamba pande zote zitajifunza mengi. Safari hii ni wanafunzi wetu watakaojifunza mengi hapa, mwakani watakuwa ni wanafunzi toka hapa watakaojifunza mengi kule Würzburg. Ni lazima tutafute wafadhili watakaosaidia gharama za safari hiyo.

Kawaida tutalazimika kuwasiliana kwa Kiingereza, lugha ambayo si rahisi kwa pande zote. Lakini nadhani tukizungumza pole pole na kutumia mikono na miguu yetu kama msaada, tutafanikiwa tu.

Nasema tena asante sana. Kama zawadi kwa VETA -Idara ya maarifa ya nyumbani na hoteli tumewaleeteni seti ya vyuma na vifaa vya jikoni, ambavyo Profesa Mehling atawakabidhi sasa.

Asante sana kwa maandalizi na mapokezi mazuri!